Aug 25, 2018 06:45 UTC
  • Tume ya Uchaguzi DRC yamzuia Bemba kugombea urais

Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imemzuia mpinzani Jean-Pierre Bemba kugombea urais katika uchaguzi ujao wa rais.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, tume hiyo imemzuia Bemba kwa msingi kuwa alipatikana na hatia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Machi 2018 ambapo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani na faini ya Euro 300,000 kwa kosa la kuwahonga mashahidi.

Mwezi Juni ICC iliagiza kuachiwa huru kwa masharti Bemba baada ya kufutiwa mashtaka ya makosa ya kivita na dhulma dhidi ya binadamu. Aliachiliwa huru kwa masharti ya kutozungumza na vyombo vya habari wala kuwasiliana na mashahidi katika kesi yake, akisubiri hukumu kuhusu tuhuma za kuhonga mashahidi na kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Kabla ya tangazo hilo la CENI, viongozi wa upinzani walitoa taarifa wakiituhumu serikali kuwa inalenga kuwazuia wagombea wa upinzani kugombea urais.

Taarifa iliyotiwa saini na Bemba pamoja na viongozi wa upinzani walio uhamishoni, Moise Katumbi na Felix Tshisekedi imetoa wito kwa Rais Joseph Kabila kuandaa mazingira huru ya uchaguzi.

Kwa ujumla tume ya uchaguzi imewazuia wagombea sita kati ya 25 waliojiandikisha kugombea urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 23.

 

Tags