Rais wa zamani wa Angola, Dos Santos, kustaafu siasa kikamilifu
(last modified Sat, 08 Sep 2018 01:23:46 GMT )
Sep 08, 2018 01:23 UTC
  • Rais wa zamani wa Angola, Dos Santos, kustaafu siasa kikamilifu

Rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos anatarajia kustaafu kikamilifu katika uga wa siasa leo Jumamosi na kukabidhi uongozi wa chama tawala kwa mrithi wake Rais Joao Lourenço wa nchi hiyo.

Dos Santos ambaye hali yake si nzuri kiafya, alianza kutawala Angola mwaka 1979 na aliomba kuachia ngazi kwa amani mwezi Agosti mwaka jana. Dos Santos alikubali kukabidhi madaraka kwa waziri wake wa zamani wa ulinzi, Joao Lourenço. Hata hivyo, aliendelea kushikilia uongozi wa chama tawala cha MPLA.

Leo Jumamosi, Dos Santos mwenye umri wa miaka 76, pia atakabdhi funguo za chama kwa Rais Joao Lourenço, katika mkutano wa chama.

Rais  wa Angola, João Lourenço

Hayo yanajiri wakati ambapo miezi michache iliyopita, watu wa familia ya dos Santos wameondolewa katika nafasi walizokuwa wakishikilia katika taasisi na makampuni ya serikali na pia katika chama.

Hali hii ilizua mvutano mkubwa. Rais wa zamani mwenyewe alionyesha hasira yake hadharani. "Mabadiliko ni muhimu lakini hayapaswi kufanywa kwa msimamo mkali," alisema dos Santos mwezi Disemba mwaka jana.

Pamoja na hayo mwezi Machi mwaka huu mtoto wa kiume wa rais huyo wa zamani wa Angola, alizuiwa kuondoka nchini  humo kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomuandama.

José Filomeno dos Santos anatuhumiwa kuhamisha kiasi cha dola milioni 500 za Marekani kutoka hazina ya taifa aliyokuwa akiiongoza, na kuipeleka kwenye akaunti binafsi.