Polisi ya Zimbabwe yapiga marufuku mikusanyiko mjini Harare baada ya kuenea kipindupindu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48109-polisi_ya_zimbabwe_yapiga_marufuku_mikusanyiko_mjini_harare_baada_ya_kuenea_kipindupindu
Polisi ya Zimbabwe imepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile katika mji mkuuu Harare baada ya kipindipindu kusambaa mjini humo na kuua watu wasiopungua 21 hadi sasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 13, 2018 07:41 UTC
  • Polisi ya Zimbabwe yapiga marufuku mikusanyiko mjini Harare baada ya kuenea kipindupindu

Polisi ya Zimbabwe imepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile katika mji mkuuu Harare baada ya kipindipindu kusambaa mjini humo na kuua watu wasiopungua 21 hadi sasa.

Marukufu hiyo ya polisi iliyotangazwa jana imekuja siku moja tu baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya hatari kama hatua moja ya kukabiliana na maradhi ya kipindupindu ambayo yanaonekana kuenea kwa kasi.

Charity Charamba, msemaji wa polisi ya Zimbabwe amewataka raia mjini Harare kuujiepusha na mikusanyiko ya aina yoyote ile  na kueleza kwamba, hatua hiyo imechukuliwa ili kukabiliana na maradhi ya kipindupindu. Hata hivyo msemaji huyo wa polisi hajaeleza marufuku hiyo ya mikusanyiko itadumu kwa muda gani.

Wizara ya Afya ya Zimbabwe ilitangaza jana kuwa, idadi ya watu walioaga dunia hadi sasa kwa maradhi ya kipindupindu imefikia 21 na kwamba, kiwango cha maambukizo ya ugonjwa huo kimeongezeka ambapo wanaougua maradhi hayo wamepindukia elfu tatu.

Baadhi ya wagonjwa wa kipindupindu wakiwa katika moja ya vituo vya afya mjini Harare kwa ajili ya matibabu

Marufuku ya mikusanyiko mjini Harare inatangazwa katika hali ambayo, Nelson Chamisa kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo amepanga kufanya mkutano mkubwa siku ya Jumamosi ambapo anatarajia kuapishwa kinembo, ikiwa ni wiki tatu zimepita tangu Rais Emmerson Mnangagwa aapishwe baada ya kushinda kiti cha Urais katika uchaguzi uliopita. 

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC kinachoongozwa na Nelson Chamisa kimeendelea kupinga ushindi wa Mnangagwa licha ya kuidhinishwa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.