Kiongozi wa upinzani Zimbabwe aakhirisha kula kiapo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48142-kiongozi_wa_upinzani_zimbabwe_aakhirisha_kula_kiapo
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe ameakhirisha mipango ya kushiriki katika hafla ya kujiapisha kama rais wa nchi iliyokuwa imepangwa kufanyika leo (Jumamosi) baada ya polisi kupiga marufuku mikutano na mijumuiko ya wananchi kufuatia nchi hiyo kuathiriwa na mlipuko wa kipindupindu kilichouwa watu 26 hadi sasa.
(last modified 2026-02-02T05:45:46+00:00 )
Sep 14, 2018 23:58 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Zimbabwe aakhirisha kula kiapo

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe ameakhirisha mipango ya kushiriki katika hafla ya kujiapisha kama rais wa nchi iliyokuwa imepangwa kufanyika leo (Jumamosi) baada ya polisi kupiga marufuku mikutano na mijumuiko ya wananchi kufuatia nchi hiyo kuathiriwa na mlipuko wa kipindupindu kilichouwa watu 26 hadi sasa.

Nelson Chamisa kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC amesema kuwa kulifanyika udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi wa Julai 30 yaliyompa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa. Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza kufanyika Zimbabwe tangu Robert Mugabe aenguliwe madarakani katika kile kinachotajwa kuwa ni mapinduzi ya jeshi ya mwezi Novemba mwaka jana.

Wakosoaji wa Chamisa wanamtuhumu kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kwamba, anajaribu kumuiga kioongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambaye mwezi Januari mwaka huu aliamua kujiapisha kama "rais wa watu" akipinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Raila Odinga, Kiongozi wa upinzani Kenya .

Hafla hiyo ya kula kiapo cha kimaonyesho ilikuwa imepangwa kufanywa sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 19 wa chama cha MDC katika mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika katika kitongoji cha Highfiled karibu na Glenview mjini Harare. Chama cha MDC kimesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika siku nyingine lakini katika eneo hilohilo.