WHO: Idadi ya walioaga dunia kwa kipindupindu Zimbabwe yafikia 45
Watu wasiopungua 45 wamepoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Zimbabwe wiki tatu zilizopita. Hayo yameelezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) huku likitaja aina hiyo ya mlipuko wa waba kuwa wenye kushindikana kutibika kwa aina mbalimbali za dawa.
WHO imesema kuwa kampeni ya utoaji chanjo kwa njia ya mdomo ilitarajiwa kuanza muda mfupi kwa kuwalenga watu 450,000 katika maeneo yaliyoathiriwa vikali na kipindupindu katika mji mkuu Harare. Dozi za chanjo hiyo zisizopungua laki tano zinatazamiwa kuwasili Zimbabwe leo ili kutolewa chanjo ya kwanza kwa njia ya mdomo ya kukabiliana na mlipuko huo wa kipindupindu. Ripoti ya Shirika la Afya Duniani na Wizara ya Afya ya Zimbabwe imebainisha kuwa hadi kufikia sasa jumla ya watu 45 wamega dunia, watu 6,428 wanashukiwa kuugua kipindupindu na wengine 96 wamethibitika kuambukizwa maradhi hayo huko Zimbabwe.
Karibu vifo vyote vimetokea katika mji mkuu, Harare huku mtu mmoja akiaga dunia katika wilaya ya Makoni mashariki mwa Zimbabwe na mwengine katika mji wa Masvingo katikati mwa nchi hiyo.