Wahajiri 34 waaga dunia katika bahari ya Mediterania
Wahajiri wasiopungua 34 wameaga dunia baada ya boti yao kupata hitilafu magharibi mwa bahari ya Mediterania, huku wengine 26 wakinusurika kifo. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imetangaza kuwa, wahajiri 31 wamenusurika kifo na kwamba miili ya wengine 11 ilipatikana Jumatatu wiki hii. Wahajiri wote aliokuwa wamepanda boti hiyo walikuwa ni kutoka katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara.
Helena Manelo Mwasisi wa taasisi ya Caminando Fronteras amesema kuwa, gadi ya ulinzi wa pwani ya Uhispania ilimpigia simu mapema jana baada ya kuwasiliana na nahodha wa boti hiyo ambapo walikuwa wakiomba msaada baada ya boti yao kukumbwa na hitilafu.
Manelo amesema kuwa, Morocco na Uhispania zinashirikiana kwa karibu katika ngazi ya usalama katika kuisaka mitandao inayojihusisha na magendo ya binadamu na kwamba Hata hivyo nchi hizo hazichukui hatua za ziada ili kunusuru maisha ya wahajiri baharini.