Mnangagwa: Kodi mpya inahitajika kwa ajili ya kufufua uchumi
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema kuwa kodi mpya kwa malipo ya kielektroniki iliyotangazwa nchini humo inaumiza lakini ni sehemu muhimu ya jitihada za serikali za kufufua uchumi.
Hayo ni matamshi ya kwanza kutolewa na Rais wa Zimbabwe tangu kutangazwa kodi hiyo mpya kwa malipo ya kielektroniki wiki iliyopita, suala ambalo limeibua malalamiko ya wananchi.
Baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa mwezi Julai mwaka huu uliodaiwa na upinzani kuwa uligubigwa na udanganyifu, Rais Mnangagwa anajaribu kuurejesha uchumi wa Zimbabwe katika mkondo sahihi. Uchumi huo ulidorora katika kipindi cha karibu miongo minne ya utawala wa Rais Mugabe ambao ulihitimishwa kwa mapinduzi ya jeshi mwezi Novemba mwaka jana.
Mthuli Ncube Waziri wa Fedha wa Zimbabwe tarehe Mosi mwezi huu alitangaza kodi hiyo mpya ya asilimia mbili akisema kuwa fedha zitakazokusanywa zitatumika katika sekta za barabara, afya na elimu. Kodi hiyo mpya itatumika katika miamala ya kibiashara ya njia ya simu na kadi na pia ile ya uhamishaji fedha kwa njia ya benki wa zaidi ya dola kumi.