Machafuko yachachamaa katika visiwa vya Comoro, kadhaa wauawa
Hali ya mchafukoge imeripotiwa kushtadi nchini Comoro huku watu kadhaa wakiripotiwa kuuawa, licha ya serikali kutangaza kuwa mambo yametengamaa baada ya siku tatu za ghasia.
Mashuhuda wanasema taharuki ingali imetanda nchini humo haswa katika mji mkuu wa kisiwa cha Anjouan, Mutsumadu, huku masoko ya maduka yakisalia kufungwa, licha ya Mohamed Daoudou, Waziri wa Mambo ya Ndani hapo jana kusema kuwa hali imerejea ya kawaida.
Ingawaje serikali inasema ni watu watatu tu waliouawa katika machafuko hayo yaliyoripuka Jumatatu iliyopita, lakini duru za habari zinasema waliouawa ni zaidi ya idadi hiyo iliyotangazwa na serikali.
Hapo jana, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) zilitoa mwito kwa pande zinazohasimiana kutochukua hatua ambazo zinaweza kufanya machafuko hayo yaongezeke na kutaka kuanzishwa mazungumzo ya amani mara moja.
Eneo la Anjouan ambalo wakazi wake wengi ni wapinzani wa Rais Azali Assoumani wa visiwa vya Comoro, liliwekewa marufuku ya kutoka nje nyakati za usiku baada ya kushuhudia miezi kadhaa ya makabiliano kati ya askari wa nchi hiyo na wafuasi wa chama cha upinzani cha Juwa, kinachoongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdallah Sambi.

Mwezi Julai mwaka huu, Rais Assoumani alishinda kura ya maoni ya kurefusha kipindi cha uongozi wa rais na kukomesha mfumo wa kuongoza kwa zamu baina ya visiwa vitatu vikuu vinavyounda Jamhuri ya watu wa Comoro.
Kura hiyo ya maoni iliyosusiwa na upinzani sasa inamruhusu Rais Azali Assoumani kugombea tena kwa vipindi vingine viwili vya miaka mitano mitano kuanzia uchaguzi uliopangwa kufanyika mapema mwakani badala ya kuondoka madarakani baada ya kipindi chake cha sasa kumalizika mwaka 2021.