Juhudi za kurejesha amani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49506-juhudi_za_kurejesha_amani_nchini_libya
Jitihada za kurejesha amani huko Libya zinaendelea kufanywa wakati huu ambapo nchi hiyo inasumbuliwa mgogoro na changamoto nyingi. Hadi sasa kumefanyika mikutano kadhaa ya kujadili njia za kurejesha amani nchini humo ukiwemo ule wa siku mbili nchini Italia uliodhuhuriwa na pande kuu husimu katika mgogoro wa ndani wa nchi hiyo na jumbe kutoka nchi 30 duniani.
(last modified 2025-10-18T09:08:01+00:00 )
Nov 14, 2018 12:03 UTC
  • Juhudi za kurejesha amani nchini Libya

Jitihada za kurejesha amani huko Libya zinaendelea kufanywa wakati huu ambapo nchi hiyo inasumbuliwa mgogoro na changamoto nyingi. Hadi sasa kumefanyika mikutano kadhaa ya kujadili njia za kurejesha amani nchini humo ukiwemo ule wa siku mbili nchini Italia uliodhuhuriwa na pande kuu husimu katika mgogoro wa ndani wa nchi hiyo na jumbe kutoka nchi 30 duniani.

Ajenda kuu ya mkutano huo lilikuwa suala la kurejesha utulivu huko Tripoli mji mkuu wa Libya, jinsi ya kuitisha mkutano mkubwa wa kitaifa utakaozishirikisha pande na makabila mbalimbali ya Libya na kubuni mpango wa kufufua uchumi wa nchi hiyo kupitia njia ya kuimarisha taasisi muhimu za nchi hiyo kama Benki Kuu na Shirika la Taifa la Mafuta.  

Giuseppe Conte Waziri Mkuu wa Italia ambaye amehutubia mkutano huo amezungumzia jinsi jamii ya kimataifa inavyopasa kuheshimu mamlaka ya kujitawala Libya na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa: Tunapaswa kuwa na matumaini ya mustakbali mwema kuhusiana na Libya na kwa msingi huo mkutano wa amani ya Libya unapasa kutumiwa kwa ajili ya kusaidia jitihada za kusitisha vita mjini Tripoli na kuunda chombo cha kujadili utekelezaji wa kanuni mpya za masuala ya usalama nchini humo. 

Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia

Mkutano huo umefanyika huku Libya ikiendelea kugubikwa na mizozo na hitilafu kati ya makundi ya kisiasa yanayowania kushika hatamu za uongozi nchini humo. Nchi hiyo ilitumbukia katika machafuko ya ndani zaidi ya miaka sita iliyopita baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi. Kuwepo nchini humo makundi ya kigaidi khususan kundi la Daesh kumeifanya hali ya kiuchumi ya Libya kuwa mbaya zaidi huku serikali za nchi ajinabi zikizidi kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Sambamba na hayo nchi za kigeni zimeendelea kuchochea moto wa vita na hitilafu nchini Libya na kugombania fusra na kudhibiti mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Gavana wa Benki Kuu ya Libya, Sadiq al Kabir amesema  changamoto za sasa nchini Libya zinatokana na hali ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi inayotawala nchi hiyo tangu mwaka 2011 na kusema kuwa: Mapigano  yanayojiri nchini humo husababisha hasara ya dola bilioni 48 na milioni 600 kila mwaka kwa uchumi wa nchi hiyo. 

Mgogoro na mauaji yanayoendelea sasa nchini Libya, hatari ya kuongezeka harakati za kigaidi na kupanuka harakati hizo katika eneo la kaskazini mwa Afrika na pia kuendelea mgogoro wa wahajiri kutoka Libya kuelekea Ulaya yote hayo si tu kuwa yamewafanya Walibya, nchi jirani na jamii ya kimataifa watake kuhitimishwa mgogoro wa ndani nchini Libya kupitia mazungumzo. Pamoja na hayo yote, hadi sasa hakujafikiwa muafaka wowote kuhusu namna uchaguzi utakavyofanyika huko Libya. 

Jenerali Khalifa Haftar anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Libya haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya mfumo wa kidemokrasia. Hata hivyo Ghassan Salame Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo anamiini kuwa: Libya ni mhanga wa madola kigeni yanayotaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na makundi mbalimbali ya nchi hiyo yanapasa kujiepusha kuomba misaada kwa madola ya nje. 

Jenerali Khaifa Haftar wa Libya 

Japokuwa hali ya sasa ya kisiasa ya Libya inayavunja moyo makundi mbalimbali ya nchi hiyo juu ya uwezekano wa  kufanyika uchaguzi nchini humo katika siku chache zijazo, lakini inaonekana kuwa njia inayoweza kuifikisha meli iliyokumbwa na dhoruba ya Libya kwenye pwani ya amani na salama ni kufikiwa mapatano kati ya makundi hayo, kukata uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, kuunda jeshi moja lenye nguvu  na kuandaa mazingira tulivu na ya amani kwa ajili ya kufanyika uchaguzi ulio huru na wa utulivu.