Baraza la Usalama la UN laifutia vikwazo Eritrea
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeifutia vikwazo Eritrea kufuatia kusainiwa makubaliano ya amani ya kihistoria kati ya nchi hiyo na Ethiopia na kuboreka uhusiano baina yake na Djibouti pia.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatano lilipiga kura na kupasisha azimio lililopendekezwa na Uingereza na kwa utaratibu huo kuifutia Eritrea vikwazo vya silaha, marufuku ya safari, kuachia mali za nchi hiyo zilizokuwa zimezuiliwa pamoja na kuondoa vikwazo vingine dhidi ya Eritrea.
Azimio hilo limezitaka pia Eritrea na Djibouti kuendeleza jitihada zao za kutatua hitilafu zilizopo baina ya nchi mbili hizo. Uhusiano wa nchi mbili hizo uliingia dosari baada ya wanajeshi wa Eritrea mwanzoni mwa mwaka 2008 kuingia katika eneo la kistratejia la Ras Doumeira kaskazini mwa mji wa Djibouti. Mwezi Julai uliopita Eritrea na Ethiopia zilisaini makubaliano ya amani na hivyo kuhitimisha uhsama uliodumu wa miongo miwili kati ya nchi mbili hizo.
Makubaliano hayo ya amani yamepelekea pia kuboreka uhusiano kati ya Eritrea na Djibouti. Weledi wa mambo wanaamini kuwa matukio haya yote yatapelekea kujiri mabadiliko chanya katika eneo la Pembe ya Afrika.