Serikali Zimbabwe yawaonya wapinzani wasithibutu kuandamana
Serikali ya Zimbabwe imetoa onyo kwa chama cha upinzani cha MDC kuwa kitawajibika iwapo mpango wake wa maandamano yaliyopangwa kufanyika Alhamisi wiki hii utasababisha vifo, majeruhi au uharibifu wa mali.
Onyo hilo linafuatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti Mosi na kusababisha vifo vya watu sita na uharibifu wa mali.
Kiongozi wa MDC Nelson Chamisa amesema wafuasi wa chama chake wataandamana ili kushinikiza kuundwa kwa serikali ya mpito, akidai kuwa rais Mnangagwa yuko madarakani kinyume cha sheria
Katibu mkuu wa idara ya mawasiliano ya Ikulu ya Zimbabwe George Charamba amesema, serikali haina nia ya kuondoa haki ya kikatiba ya wananchi kufanya maandamano na kuongeza kuwa, kuna maeneo yanayolindwa ambayo waandamanaji hawataruhusiwa kuingia.
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe aliapishwa mwezi Agosti na kutoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya vyama vya siasa kwa ajili ya kujenga upya uchumi wa nchi hiyo.
Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF alishinda kwa kupata asilimia 50.8 ya kura huku mgombea wa chama cha MDC, Nelson Chamisa akipata asilimia 44.3 ya kura katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi Julai.
Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza wa Rais nchini Zimbabwe baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ambaye alilazimishwa na jeshi kuondoka madarakani.