Makumi ya watu wauawa wakipigania dhahabu nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50873-makumi_ya_watu_wauawa_wakipigania_dhahabu_nchini_chad
Makumi ya watu wameuawa katika mapigano baina ya wanamgambo wa Chad na Sudan katika mgodi wa dhahabu kaskazini mwa Chad.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 15, 2019 02:42 UTC
  • Makumi ya watu wauawa wakipigania dhahabu nchini Chad

Makumi ya watu wameuawa katika mapigano baina ya wanamgambo wa Chad na Sudan katika mgodi wa dhahabu kaskazini mwa Chad.

Sheikh Twahir, mwanachama wa genge la wanamgambo wa Chad la CCMSR amesema wapiganaji wa kundi la Sudanese Movement for Justice and Equality (MJE) waliwashambulia katika maeneo yao ya kuchimba dhahabu na ndipo wakalazimika kujibu mapigo, ambapo makumi ya watu wameuawa.

Duru za kiusalama nchini Chad zimearifu kuwa, wanamgambo wa Sudan waliingia nchini humo wakitokea Libya na kushambulia machimbo ya dhahabu ya wapiganaji wa Chad, ambapo idadi kubwa ya watu wameuawa katika makabiliano hayo yaliyotokea kati ya Jumamosi na Jumapili. 

Wachimba Chad

Mara nyingi wachimba migodi kutoka maeneo mengine ya Chad na wengine kutoka nchi jirani ya Sudan wanavamia maeneo ya dhahabu kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka.

Hata hivyo wenyeji wa eneo hilo wanasema kuwa, dhahabu hiyo ni mali yao wao na kwamba mtu yeyote kutoka eneo jingine hana haki ya kumiliki dhahabu hiyo.

Watu 30 waliuawa katika mapigano mengine kama haya mwezi uliopita wa Disemba.

Migodi mikubwa ya dhahabu iligunduliwa katika eneo hilo la kaskazini mwa Chad katika miaka ya 2012 na 2013 na jambo hilo limepelekea watu kutoka maeneo mengine ya nchi hiyo maskini, bali hata kutoka nchi jirani kumiminika katika eneo hilo kwa tamaa ya kunufaika na utajiri huo wa maliasili.