Rais wa Zimbabwe alaani ukandamizaji maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51048-rais_wa_zimbabwe_alaani_ukandamizaji_maandamano
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amelaani vikosi vyake vya usalama kwa kutumia mabavu kukandamiza maandamano ya wananchi waliokuwa wakilalamikia ughali ya maisha.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 22, 2019 14:52 UTC
  • Rais wa Zimbabwe alaani ukandamizaji maandamano

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amelaani vikosi vyake vya usalama kwa kutumia mabavu kukandamiza maandamano ya wananchi waliokuwa wakilalamikia ughali ya maisha.

Akizungumza Jumanne, Mnangagwa ameahidi kufanya uchunguzi kuhusu ukatili uliotumiwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji hao ambao wanapinga serikali yake.

Akizungumza baada ya kukatiza safari yake nchini Uswisi na kurejea nyumbani, Mnangagwa amesema mabavu yaliyotumiwa na polisi dhidi ya waandamanaji hayakubaliki na ni usaliti kwa 'Zimbabwe mpya."

Ameonya kuwa watakaopatikana na hatia katika uchunguzi huo watafutwa kazi huku akiitisha mazungumzo ya kitaifa ambayo yatajumuisha makanisa, jumuiya za kiraia na wapinzani.

Maafisa wa usalama Zimbabwe wakikabiliana na waandamanaji

Kwa siku kadhaa sasa nchini Zimbabwe, wananchi  wameandamana kupinga ongezeko la bei ya mafuta. Hadi sasa watu watatu wamepoteza maisha kwenye mapambano huku maduka kadhaa yakiporwa na baadhi ya nyumba kubomolewa.