Wahajiri 30 wafa maji baada ya boti kuzama pwani ya Djibouti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51219-wahajiri_30_wafa_maji_baada_ya_boti_kuzama_pwani_ya_djibouti
Maiti 30 zimepatikana zikielea majini baada ya boti mbili zilizokuwa zimebeba makumi ya wahajiri kuzama katika pwani ya Djibouti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2019 11:04 UTC
  • Wahajiri 30 wafa maji baada ya boti kuzama pwani ya Djibouti

Maiti 30 zimepatikana zikielea majini baada ya boti mbili zilizokuwa zimebeba makumi ya wahajiri kuzama katika pwani ya Djibouti.

Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limetangaza leo kuwa, wapiga mbizi wa Gadi ya Pwani ya nchi hiyo waliipata miili ya wahajiri hao katika eneo la Godoria kaskazini mashariki mwa Djibouti.

Kijana wa miaka 18 ambaye ni mingoni mwa manusura wa ajali hiyo ameliambia shirika hilo la kushughulikia wahajiri la Umoja wa Mataifa kuwa, boti yao ambayo ilikuwa imebeba watu 130 wakiwemo wanawake 16 ilizama muda mfupi baada ya kuanza safari.

Lalini Veerassamy, Mkuu wa IOM nchini Djibouti amesema tukio hilo la kuhuzunisha limeweka wazi namna wahajiri wanavyokumbana na hatari mbalimbali wanapokuwa katika safari hatarishi za baharini.

 

Wahajiri wa Kiafrika wakiokolewa katika bahari ya Mediterania

Inaarifiwa kuwa, wahajiri hao ni raia wa nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika, ambao walikuwa katika safari hiyo hatarishi kwenda Ulaya kutafuta maisha. Hata hivyo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu boti ya pili iliyozama katika ajali hiyo ya jana Jumanne.

Mapema mwezi huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilitangaza kuwa wahajiri 2,262 wameaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka ulioisha wa 2018, licha ya mwaka huo kushuhudia kupungua wimbi la wahajiri kuelekea barani Ulaya.