Upinzani Nigeria: Kuakhirishwa uchaguzi ni njama za kumbakisha Buhari madarakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51592-upinzani_nigeria_kuakhirishwa_uchaguzi_ni_njama_za_kumbakisha_buhari_madarakani
Chama kikuu cha upinzani nchini Nigeria kimetilia shaka uamuzi wa Tume ya Uchaguzi wa kuakhirisha uchaguzi, kikisisitiza kuwa kitendo hicho ni hatari kwa taifa na kina lengo la kuandaa mazingira ya kuiba kura kwa maslahi ya rais wa sasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 16, 2019 12:45 UTC
  • Upinzani Nigeria: Kuakhirishwa uchaguzi ni njama za kumbakisha Buhari madarakani

Chama kikuu cha upinzani nchini Nigeria kimetilia shaka uamuzi wa Tume ya Uchaguzi wa kuakhirisha uchaguzi, kikisisitiza kuwa kitendo hicho ni hatari kwa taifa na kina lengo la kuandaa mazingira ya kuiba kura kwa maslahi ya rais wa sasa.

Uche Secondu, Mwenyekiti wa chama cha People’s Democratic Party (PDP) amesema hatua hiyo ni hatari kwa demokrasia ya nchi hiyo, na ni jambo lisilokubalika.

Amebainisha kuwa, "hii ni sehemu ya njama za Buhari za kuendelea kung'angania madaraka, ilhali anajua kuwa wananchi hawamtaki tena."

Wakati huohuo, chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kimetoa taarifa kikieleza pia kughahabishwa kwake na hatua hiyo ya kuakhirishwa uchaguzi huo.

Mahmood Yakubu, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) ametoa tangazo la ghafla la kuakhirisha uchaguzi huo kwa muda wa wiki moja, masaa machache kabla ya wananchi wa Nigeria kuelekea katika masanduku ya kupiga kura kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia hii leo.

Rais Buhari (kushoto) na Atiku Abubakar

Amesema uchaguzi huo umeakhirishwa kwa sababu za changamoto za kilojistiki, akisisitiza kuwa tume hiyo ina nia ya kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.

Katika uchaguzi huo ambao sasa utafanyika Februari 23, Rais wa sasa Muhammadu Buhari anayewania muhula wa pili, atachuana na wagombea wengine 72, ingawaje mfanyabiashara Atiku Abubakar wa chama cha upinzani cha PDP ndiye anayetazamiwa kumtoa kijasho Buhari katika kinyang'anyiro hicho.