Raia 17 wauawa katika shambulizi jipya lililotokea katikati ya Mali
Duru za usalama nchini Mali zimetangaza habari ya kuuawa raia 17 katika eneo la katikati mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Duru za kieneo zimethibitisha habari hiyo na kutangaza leo kuwa, mripuko huo ulitokea jana baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya mwili wa mtu mmoja aliyeuawa kwa risasi kuripuka na kupelekea watu 17 waliokuwepo kwenye shughuli hiyo ya mazishi kuuawa kigaidi katika kijiji cha Diankabou cha katikati mwa Mali.
Nchi ya Mali imekuwa katika machafuko tangu mwaka 2012 baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi na baadaye waasi kuteka maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Wanajeshi wa mkoloni Ufaransa wako nchini humo tangu mwaka 2013 lakini wameshindwa kusaidia juhudi za kurejesha amani na kupambana na vitendo vya kigaidi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mwaka jana pekee yaani 2018, zaidi ya raia 500 waliuawa katika mapigano yaliyoyakumba maeneo mbalimbali ya Mali hasa ya katikati mwa nchi hiyo.
Hali ya usalama inazidi kuwa mbaya nchini Mali siku baada ya siku. Siku chache zilizopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani shambulizi la kigaidi lililowalenga askari wa kikosi cha kulinda amani cha umoja huoMINUSMA lililotokea katika eneo la Siby na kuua askari watatu raia wa Guinea na kujeruhiwa wengine kadhaa.
Mwezi wa Januari mwaka huu pia, askari 12 wa MINUSMA, waliuliwa na wengine wasiopungua 25 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuzima shambulio la watu wenye silaha karibu na kijiji kimoja kaskazini mwa Mali.