Kimbunga Idai kimeua watu 268 Zimbabwe, mamia hawajulikani waliko
Waziri wa habari wa Zimbabwe Bibi Monica Mutsvangwa amesema, watu 268 wamethibitishwa kufariki na mamia ya wengine hawajulikani walipo kufuatia kimbunga Idai kilichoshambulia sehemu ya mashariki ya nchi hiyo katikati ya mwezi uliopita.
Mutsvangwa aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maafa yaliyosababishwa na kimbunga Idai. Amesema kazi za uokoaji zinaendelea na inakadiriwa kuwa miili zaidi ya watu waliofariki itagunduliwa.
Amesema idara husika inakarabati njia ya kwenda eneo lililokumbwa na maafa ili kuhakikisha vifaa vya uokoaji vinawafikia watu walioathiriwa na kimbunga hicho.
Kwa ujumla karibu watu 850 wamepoteza maisha katika nchi za kusini mwa Afrika za Zimbabwe, Malawi na Msumbuji kufuatia kimbunga Idai kilichosababisha mafuriko katika ukanda huo. Aghalabu ya waliofariki ni kutoka Msumbuji nchi ambayo likuwa ya kwanza kukumbwa na kimbunga hicho kutokana na kuwa iko katika Pwani ya Bahari ya Hindi.
Kufuatia hali hiyo, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa umetangaza kutoa msaada wa dola milioni 20 kusaidia waathirika.
Kwa mujibu wa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock mfuko huo wa dharura CERF umetangaza kutenga dola milioni 20 kwa ajili ya kupiga jeki msaada wa kibinadamu kufuatia Kimbunga Idai kilichokumba nchi hizo tatu za kusini mwa Afrika.
Lowcock hata hivyo amesema mgao huo kutoka kwa CERF ni wa kukabiliana na dharura za hivi sasa lakini hautoshi kuweza kukabiliana na mahitaji ambayo yanatarajiwa kuongezeka na hiyvo ametoa wito kwa wafadhili kuchangia fedha kwa ajili ya watu walioathirka kufuatia kupiga kwa kimbunga Idai.