Duru mpya ya mgogoro wa kisiasa na kijeshi nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52675-duru_mpya_ya_mgogoro_wa_kisiasa_na_kijeshi_nchini_libya
Katika hali ambayo, jamii ya kimataifa ilikuwa imeelekeza macho na masikio yake katika mkutano wa "mazungumzo ya kitaifa ya Libya" kwa ajili ya kufikia utatuzi wa kisiasa na kuvuka kipindi cha mgogoro wa sasa, mashambulio ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na kusonga mbele kuelekea mji mkuu Tripoli, yameitumbukiza nchi hiyo katika kipindi kipya cha mgogoro.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2019 21:47 UTC
  • Duru mpya ya mgogoro wa kisiasa na kijeshi nchini Libya

Katika hali ambayo, jamii ya kimataifa ilikuwa imeelekeza macho na masikio yake katika mkutano wa "mazungumzo ya kitaifa ya Libya" kwa ajili ya kufikia utatuzi wa kisiasa na kuvuka kipindi cha mgogoro wa sasa, mashambulio ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na kusonga mbele kuelekea mji mkuu Tripoli, yameitumbukiza nchi hiyo katika kipindi kipya cha mgogoro.

Vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar vimeanza mashambulio hayo chini ya operesheni ya "kurejesha heshima". Jenerali huyo mstaafu amedai kuwa, lengo la operesheni ya sasa ya kijeshi ni kurejesha usalama na sheria nchini Libya na kupambana pia na makundi ya kigaidi. Katika operesheni hiyo, vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar vimefika takriba kilomita 30 kutoka mji mkuu Tripoli yalipo makao makuu ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa.

Hali hiyo imeifanya jamii ya kimataifa kuingiwa na hofu na wasiwasi mkubwa kuhusiana na mustakabali wa Libya, kiasi kwamba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura kujadili hali ya mambo katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imevitaka vikosi vya Khalifa Hatar viache mara moja hatua yake ya kusonga mbele kuelekea mji mkuu Tripoli. Aidha Baraza la Usalama limezitaka pande hasimu nchini Libya kuendelea na mwenendo wa mazungumzo na kutekeleza ahadi zao za kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika njia ya kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi alioano kuhusiana na harakati ya kijeshi nchini Libya na kusema kuwa, Libya haiwezi kupatiwa ufumbuzi kupitia njia ya kijeshi na kwamba, njia pekee ya kuyapatia utatuzi matatizo ya nchi hiyo ni mazungumzo.

Shambulio la Jenerali Khalifa Haftar ambaye kwa sasa anaongoza serikali ya Libya yenye makao yake Tobruk mashariki mwa nchi hiyo yanafanyikka katika hali ambayo, mkutano wa "mazungumzo ya kitaifa kwa shabaha ya kuiunganisha pamoja Libya, kuandaliwa uchaguzi na kuchorwa ramani ya njia ya namna ya kurjesha amani umepangwa kufanyika tarehe 14- 16 za mwezi huu wa Aprili. Viongozi wa Libya na jamii ya kimataifa walikuwa na matumaini kwamba, mkutano ujao utaweza kuandaa mazingira ya kuhitimishwa mvutano katika nchi hiyo na kuandaa utangulizi na mazingira mwafaka ya kufanyika uchaguzi kupitia njia ya mazungumzo ya kisiasa. Lakini mashambulio ya sasa ya vikosi vya Khalifa Haftar yamevuruga mahesabu yote ya kisiasa na kijeshi ya nchi hiyo.

Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, mashambulio ya sasa ya vikosi vitiifu kwa Jenerali Haftar yametolana na kuendelea uingiliaji wa siri na wa dhahiri wa vikosi vya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya hususan kufuatia safari ya Jenerali Haftar nchini Saudi Arabia na Imarati na kwamba, mashambulio hayo yamefanyika kwa baraka kamili ya Riyadh na Abu Dhabi.

Abdulrahman Sewehli, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Uongozi la Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya, ameashiria safari ya juma lililopita ya Jenerali Khalifa Haftar huko Saudi Arabia na Imarati na kusema kuwa: Mpango wa kurejesha udikteta Libya kwa kumtumia Haftar hautafanikiwa kama ambavyo juhudi za jenerali huyo mstaafu za kuidhibiti kijeshi nchi hiyo zitafeli na kugonga mwamba.

Jenerali Khalifa Haftar

Mgogoro wa Libya umeingia katika hatua mpya na hatari na inaonekana kuwa, Jenerali Haftar amekusudia kutekeleza azma yake ya kuidhibiti Tripoli na hivyo kutimiza ndoto yake ya kukalia kiti cha uongozi nchini Libya. Hii ni katika hali ambayo, vikosi vilivyoko Tripoli navyo vimeingia katika medani ya mapambano ili kuzuia vikosi vya Haftar kusonga mbele kuuendea mji huo.

Vicent Hugeux, mhadhiri wa jiopolitiki anasema kuhusiana na jambo hili hili kwamba: Hakuna utatuzi na ufumbuzi wa kisiasa nchini Libya. Licha ya kuweko juhudi zote hizi za kidiplomasia, lakini jinamizi la Libya ni kubwa kiasi kwamba, endapo upande mmoja utafanikiwa kudhibiti mambo basi utatawala na jamii ya kimataifa itakuwa pamoja na upande huo.

Hapana shaka kuwa, siku zijazo nchini Libya zitakuwa ni zenye kuainisha hatima na mustakabali wa kisiasa wa Libya; na kuendelea mapigano ya sasa, kutapelekea kuibuka vita vya kila upande ambapo Libya itatumbukia katikam dimbwi la damu au hali hii itapelekea kuibuka mkwamo wa kisiasa na kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.