Askari 10 wauawa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi la Mali
Watu wenye silaha wameua askari wasiopungua 10 wa jeshi la Mali baada ya kushambulia kambi moja ya jeshi hilo mapema leo katika eneo la Guire katikati mwa nchi.
Askari mmoja wa jeshi hilo amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, "Ni kweli kambi yetu ya Guire imeshambuliwa asubuhi ya leo mwendo wa saa kumi na moja alfajiri na wavamizi waliokuwa wamebeba silaha wakiwa juu ya pikipiki. Walituvamia wakitokea katika msitu wa karibu."
Mashuhuda wanasema kuwa, baada ya magaidi hao kutekeleza shambulizi hilo, waliweka pikipiki zao juu ya gari la kijeshi na kuondoka nalo.
Ingawaje hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini katika miaka ya karibuni, wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda wamekuwa wakifanya mashambulizi katika eneo hilo la katikati mwa Mali.

Mwezi uliopita, watu zaidi ya 130 waliuawa baada ya wavamizi waliobeba silaha kushambulia kijiji cha watu wa kabila la Fulani katika eneo la Ogossagou katikati mwa Mali, wiki moja baada ya askari 16 wa jeshi la nchi hiyo kuuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi huko Mopti katikati mwa nchi.
Licha ya askari 4,500 wa Kifarasa kuwepo katika eneo la Sahel mwa Afrika tangu mwaka 2013, lakini mashambulizi ya kigaidi yameshika kasi katika eneo hilo.