Rais wa muda wa Algeria ataka kuweko mazungumzo ya kitaifa
Abdelkader Bensalah, Rais wa Muda wa Algeria ametoa wito wa kuweko mazungumzo ya kitaifa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwa shabaha ya kufikia mwafaka katika masuala ambayo yamezusha hitilafu nchini humo.
Abdelkader Bensalah, sambamba na kusisitiza kwamba, uchaguzi wa Rais nchini Algeria utafanyika katika muda uliopangwa yaani tarehe 4 Julai mwaka huu ametaka kuweko mazungumzo ya kitaifa baina ya makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo.
Amesema kuwa, kuna haja ya kuweko mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi ya kiraia na kisiasa kwa ajili ya kujadili mazingira mwafaka kwa ajili ya kufanyika uchaguzi ujao.
Wito huo unatolewa katika hali ambayo, wananchi wa Algeria wameendelea na maandamano yao ya kupinga serikali ya mpito ya nchi hiyo na kuishutumu kuwa inapoteza muda.
Wapinzani wanaamini kwamba wakati wa kufanyika uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia nchini Algeria haujafika kwani kuna mambo mengi ya kurekebishwa na kuna mianya mingi ya kuzibwa kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Maandamano ya miezi kadhaa ya raia wa Algeria waliokuwa wakipinga tangazo la Rais Abdelaziz Bouteflika la kutaka kugombea tena kwa muhula wa tano mfululizo kwenye uchaguzi wa rais, hatimaye yalimlazimisha rais huyo sambamba na kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, ajiuzulu pia uongozi wa nchi.