Algeria yawakamata wahamiaji haramu 95
Vikosi vya usalama Algeria vimewakamata wahamiaji haramu 95 kwenye operesheni mbalimbali.
Wizara ya ulinzi ya Algeria imetoa taarifa na kusema askari walioko kwenye mkoa wa pwani Oran, kilomita 400 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Algiers, wamezuia jaribio la usafirishaji haramu wa watu 18 kwa njia ya boti.
Kwenye operesheni nyingine, jeshi la Algeria limewakamata wahamiaji haramu 63 kutoka mataifa tofauti mkoani Tlemcen, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo inayopakana na Morocco. Zaidi na hayo, jeshi lake limewakamata wahamiaji haramu wengine 14 mkoani Tamanrasset, kusini mwa nchi hiyo.
Hayo yanajiri siku moja baada ya Gadi ya Pwani ya Libya kutangaza kuwaokoa takribani wahamiaji haramu wapatao 150 waliokuwa kwenye boti katika Bahari ya Mediterania wakielekea Ulaya. Aidha serikali ya nchi jirani ya Tunisia imetangaza kuwa wahajiri 70 waliaga dunia katika ajali ya Ijumaa katika pwani ya Tunisia.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilitangaza kuwa zaidi ya wahajiri elfu mbili waliaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka uliopita wa 2018.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.