Wamalawi watakiwa watulie, matokeo ya uchaguzi kutangazwa wiki ijayo
Tume ya uchaguzi ya Malawi imetoa mwito wa kuwepo utulivu na uvumilivu miongoni mwa wananchi, wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea baada ya uchaguzi wa Jumanne.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Jane Ansah, amesema matokeo kutoka kwenye majimbo yameanza kufikia kwenye kituo kikuu cha kuhesabia kura, lakini yanatakiwa kuthibitishwa kabla ya kutangazwa. Amesema hakuna njia ya mkato zaidi ya kuhesabu kura na kuwataka Wamalawi waonyeshe uvumilivu wakati huu kura zinapohesabiwa.
Pia amewatahadharisha wananchi kuwa makini na mitandao ya kijamii, ambayo inatoa matokeo ya uchaguzi, na kusema licha ya kuwa baadhi inasema ukweli, mingine inasema uongo na inaweza kusababisha vurugu. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Malawi, matokeo yanatakiwa kutangazwa katika kipindi cha siku nane baada ya upigaji kura kufanyika. Mbali na uchaguzi wa rais, wananchi wa Malawi pia waliwapigia kura wabunge na madiwani.
Wananchi wa Malawi jana walijitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ambapo Rais Peter Mutharika alikabiliwa na ushindani mkali. Mutharika, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2014, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa naibu wake Saulos Chilima na mhubiri wa zamani wa Lazarus Chakwera.
Chilima mwenye umri wa miaka 46 na ambaye ni mkuu wa zamani wa kampuni ya mawasiliano, alijiondoa kwenye chama cha Mutharika Democratic Progressive Party mwaka uliopita na akaanzisha chama chake ili kushindana na Mutharika.
Naye Chakwera ambaye ana umri wa miaka 64 alishindwa na Mutharika katika uchaguzi uliopita mwaka 2014 na ili kuimarisha nafasi yake ya ushindi, mara hii amejiunga na rais aliyekuwa mtangulizi wa Mutharika Joyce Banda.