Wananchi Algeria waendelea na maandamano; wataka kukabidhiwa madaraka kwa amani
Maelfu ya wananchi wa Algeria jana Ijumaa waliendelea kuandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Algiers na katika miji mingine ya nchi hiyo wakitaka kukabidhiwa kwa amani madaraka nchini.
Waliandamana katika mji mkuu Algiers na katika miji mingine ya nchi hiyo huku wakipiga nara za kusisitiza kuondolewa katika marhala ya kukabidhi madaraka viongozi wa serikali iliyopita ya Rais Abdelaziz Bouteflika. Wafanya maandamano hao walikusanyika katika maidani ya al Barid inayotambulika kama maidani kuu zaidi katika mji mkuu Algiers. Wametaka pia kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa baadhi ya viongozi wa utawala uliopita ambao walitajwa kuwa mafisadi.
Maandamano hayo ya jana ni maandamano ya Ijumaa ya 14 kufanyika huko Algeria. Algeria hivi sasa inashuhudia mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo, mabadiliko ambayo ni natija ya maandamano mtawalia ambayo yamekuwa yakifanywa na Waalgeria tangu Februari 22 mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa wananchi wa Algeria walikuwa wakilalamikia hatua ya rais wa zamani wa nchi hiyo kugombea kwa muhula wa tano mtawalia. Maandamano yalishtadi nchini humo kupinga hatua hiyo na hatimaye Bouteflika akalazimika kujiuzulu kiti cha urais.