Wananchi wa Malawi kusubiri zaidi kujua matokeo ya uchaguzi wa rais
Mahakama nchini Malawi imeiamuru Tume ya Uchaguzi nchini humo kutotangaza matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni, kufuatia malalamiko ya wizi wa kura yaliyotolewa na upinzani.
Katika agizo hilo, Mahakama Kuu imetaka kusitishwa utangazaji wa matokeo ya kura ya rais na kutoa maelekezo ya kuhesabiwa upya kwa kura za theluthi ya maeneo yaliyoshiriki uchaguzi. Tume ya uchaguzi nchini humo ilisimamisha kutangaza matokeo hayo baada ya kupokea malalamiko 147 kutoka kwa baadhi ya vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo wa Jumanne iliyopita.
Chama kikuu cha upinzani cha Malawi Congress (MCP) kinachoongozwa na Lazarus Chakwera, kiliwasilisha malalamiko mahakamani juu ya kile kilichodai kuwa makosa yaliyojitokeza katika wilaya 10 kati ya 28 nchini humo.
Malalamiko hayo yamewasilishwa licha ya timu ya waangalizi ya Umoja wa Ulaya kusisitiza kuwa uchaguzi huo ulisimamiwa vizuri, ulikuwa na uwazi pamoja na ushindani mkali.

Wananchi wa Malawi Jumanne iliyopita ya Mei 22 walijitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ambapo Rais Peter Mutharika alikabiliwa na ushindani mkali.
Mutharika ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2014, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa naibu wake Saulos Chilima na mhubiri wa zamani Lazarus Chakwera.