ICC yazitaka nchi wanachama kutekeleza hati za kukamatwa Netanyahu, Gallant
Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Fadi El Abdallah ameiambia kanali ya Al-Jazeera kwamba, nchi wanachama wa Mkataba wa Roma zina wajibu wa kisheria kushirikiana na mahakama hiyo katika kutekeleza waranti wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wa Vita wa utawala huo pandikizi, Yoav Gallant.
"Tunahitaji kuona ushirikiano mpana kutoka kwa nchi wanachama katika kutekeleza amri hizi za kukamatwa (wawili hao)," El Abdallah amesema, akitoa wito wa kuongezeka kwa dhamira ya kimataifa ya kutekelezwa haki.
ICC ilitoa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant mnamo Novemba 21, 2024, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Aidha wawili hao wanaandamwa na mashitaka ya kusababisha, kurefusha au kushajiisha vita vya mauaji ya halaiki vilivyoanza Octoba 2023 huko Gaza, ambavyo hadi sasa vimeua zaidi ya Wapalestina 67,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya ICC, mashtaka dhidi yao yanatokana na vitendo vilivyofanywa kati ya Oktoba 8, 2023, na Mei 20, 2024. Mahakama hiyo imesema kuna "ushahidi wenye mashiko na wa kuaminika" kwamba Netanyahu na Gallant waliwazuia kwa makusudi wakazi wa Gaza kufikiwa na rasilimali muhimu kwa ajili ya kuishi.
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) waliamua hivi karibuni kwamba, hati zilizotolewa na korti hiyo ya mjini The Hague za kukamatwa Netanyahu naGallant zingali na itibari, huku wakikaidi mashinikizo makubwa ya Israel na Marekani ya kufutulia mbali waranti hizo.
Haya yanaripoti huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uhispania, Fernando Grande-Marlaska akisema kuwa, hatua za kisheria huenda zikachukuliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Israel baada ya utawala wa Kizayuni kuvamia raia wa Uhispania waliokuwemo kwenye msafara wa Sumud au Global Sumud Flotilla uliokuwa unajaribu kuwafikishia msaada wananchi wa Gaza.