Wanafunzi Algeria wakataa kufanya mazungumzo na utawala ulioko madarakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54070-wanafunzi_algeria_wakataa_kufanya_mazungumzo_na_utawala_ulioko_madarakani
Wananfunzi nchini Algeria jana walifanya maandamano katika mitaa mbalimbali ya Algiers mji mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuwa hawatafanya mazungumzo na utawala ulioko madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2019 03:04 UTC
  • Wanafunzi Algeria wakataa kufanya mazungumzo na utawala ulioko  madarakani

Wananfunzi nchini Algeria jana walifanya maandamano katika mitaa mbalimbali ya Algiers mji mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuwa hawatafanya mazungumzo na utawala ulioko madarakani.

Maelfu ya wanafunzi na walimu wao kama ilivyokuwa katika wiki zilizopita jana Jumanne walifanya maandamano makubwa katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu Algiers huku wakipiga nara ya kupinga kufanya mazungumzo na rais wa muda wa nchi hiyo. Rais wa muda wa Algeria ndiye aliyetoa wito wa kufanya mazungumzo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Wanafunzi hao ambao walimiminika kwa wingi katika mitaa ya Algiers katika Jumanne nyingine ya 16 mtawalia walikuwa wakipiga nara za "hatufanyi mazungumzo na timu iliyoko madarakani" na "Bin Saleh si rais wa nchi." 

Wafanya maandamano wametaka kufanyika uchaguzi haraka iwezekanavyo. Algeria imetumbukia katika mgogoro mkubwa  wa kisiasa tangu kuanza maandamano nchini humo Februari 22 mwaka huu. Abdel Qadir bin Saleh ambaye tarehe Tisa Aprili alichaguliwa kuwa Rais wa muda wa Algeria kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo wiki moja baada ya kujiuzulu Rais Abdelaziz Bouteflika tarehe Sita mwezi huu wa Juni alitoa wito akiwaalika wapinzani kuketi pamoja kwenye meza ya mazungumzo ili kuzungumzia suala la kufanyika uchaguzi mpya wa rais nchini humo. 

Abdel Qadir bin Saleh, Rais wa muda wa Algeria 
 

Ingawa kwa mujibu wa katiba ya Algeria bin Saleh anapasa kuondoka madarakani ifikapo tarehe Tisa mwezi Julai lakini yeye ametangaza kuwa ataendelea kukalia kiti hicho hadi hapo atakapochaguliwa rais mpya kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na katiba.