Jun 17, 2019 12:36 UTC
  • Watu 30 wauawa katika hujuma za kigaidi wakitizama mpira Nigeria

Watu wasipungua 30 wameuawa katika mashambulizi kaskazini mwa Nigeria katika hujuma inayoaminika kutekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa taarifa, magaidi watatu waliokuwa wamejifunga mikanda ya mabomu walijilipua Jumapili usiku katika eneo la Konduga, kilomita 38 kutoka mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguru. Taarifa  zinasema magaidi hao walijilipua katika ukumbi wakati watu walipokuwa wakitizama mechi ya soka kwa njia ya televisheni. Mkuu wa opareseheni za dharura nchini Nigeria Usman Kachalla amewaambia waandishi habari leo kuwa, watu wengin 40 walijeruhiwa katika tukio hilo.

Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kisha kuenea hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.B

Hadi sasa mashambulio hayo yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini na tano kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haramu, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo, na hivyo kukabiliwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Tags