Kuendelea uingiliaji wa kigeni nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55094-kuendelea_uingiliaji_wa_kigeni_nchini_sudan
Huku mgogoro wa kisiasa ukiendelea nchini Sudan, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo umeongezeka kwa kadiri kwamba baadhi ya nchi za eneo zikiongozwa na Saudi Arabia zinafuatilia kwa nguvu zao zote suala la kuwa na ushawishi mkubwa katika nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2019 23:09 UTC
  • Kuendelea uingiliaji wa kigeni nchini Sudan

Huku mgogoro wa kisiasa ukiendelea nchini Sudan, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo umeongezeka kwa kadiri kwamba baadhi ya nchi za eneo zikiongozwa na Saudi Arabia zinafuatilia kwa nguvu zao zote suala la kuwa na ushawishi mkubwa katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Katika uwanja huo, Ibrahim Othman al-Umair, mwambata wa kijeshi wa Saudia nchini Sudan alikutana na kuzungumza hivi karibuni mjini Khartoum na Muhammad Othman al-Hussein, Kamanda mpya wa Majeshi ya Sudan.

Katika mazungumzo hayo, al-Hussein alisema kuwa uhusiano wa Saudia na Sudan ni 'uhusiano maalumu na ulio imara' na kumshukuru mwambata huyo wa Saudia kwa kuchangia katika uimarishwaji wa uhusiano huo.

Matamshi ya kamanda mpya huyo wa majeshi ya Sudan kuhusiana na kuimarika uhusiano wa nchi hiyo na Saudia yametolewa katika hali ambayo Wasudan katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakifanya maandamano katika miji tofauti ya nchi hiyo kulalamikia uingiliaji unaofanywa nchini humo na nchi za Saudia, Imarati na Misri.

Swadiq al-Mahdi, Kiongozi wa chama cha Umma cha Sudan huku akitahadharisha kuhusu uingiliaji unaofanywa na nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo amesema: Sudan inakabiliwa na changamoto ya uingiliaji wa kigeni. Wao hawaitakii mema Sudan na wanataka nchi hii isiwe mfano wa mwamko kwa mataifa mengine.

Imarati pia inatuhumiwa kuingilia mambo ya ndani ya Sudan

Uingiliaji wa kigeni katika masuala ya Sudan uliingia katika hatua mpya kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya serikali ya Rais Omar al-Bashir mwezi Aprili uliopita, ambapo liliunda Baraza la Kijeshi kwa ajili ya kuendesha mambo ya nchi hiyo. Saudia, Imarati na Misri ni nchi tatu za Kiarabu zinazounga mkono Baraza la Kijeshi la Sudan, kwa lengo la kujidhaminia maslahi yao binafsi na kujiandalia nafasi ya kuwa na ushawishi katika uendeshaji wa mambo ya nchi hiyo.

Katika uwanja huo, kuendelea uwepo wa kijeshi wa Sudan katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen kuna umuhimu mkubwa kwa utawala wa Riyadh, ambao uko tayari kuwapa fedha na silaha viongozi wa kijeshi wa Baraza la Kijeshi la Sudan kwa madhumuni ya kuwashawishi waendelee kubakisha askari wao katika muungano huo wa kijeshi. Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, hivi sasa Sudan ina askari na mamluki wapatao elfu 30 katika vita vya Yemen ambapo wengi wao ni watoto wadogo wanaotoka katika maeneo masikini ya Sudan kama vile Darfur, ambao huhatarisha maisha yao katika vita hivyo ili kupata kiasi kidogo cha pesa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imekiri kuhusu hatua ya kikosi cha Rasiamali ya Haraka ya Sudan ya kutuma watoto wadogo wa nchi hiyo katika vita vya Yemen na kusema, wakuu wa kikosi hicho wamebadilisha nyaraka za utambulisho za watoto waliotumwa kama askari wapiganaji katika muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen.

Askari wa Sudan waliotumwa kupigana nchini Yemen kwa malipo ya Saudia

Kwa kutilia maanani matukio ya Sudan, hivi sasa vyama vingi vya siasa na watu wa Sudan hawataki tena kuwepo kijeshi kwa raia wa nchi hiyo katika muungano wa kijeshi wa Saudia huko Yemen na wanataka askari wa nchi hiyo waondeke katika muungano huo mara moja na kurejea nyumbani. kwa mtazamo wao, kuendelea kuwepo kijeshi Sudan katika muungano huo unaoongozwa na Saudia na Imarati nchini Yemen kunazinyooshea njia Riyadh na Abu Dhabi ili ziendelee kuzidisha uingiliaji wao katika mambo ya Sudan, na hivyo kutumiwa vibaya fedha na nguvukazi ya nchi hiyo.

Kuendelea kwa mwenendo huo wa Sudan kunatia wasiwasi mkubwa. Kwa kuendelea kuliunga mkono Baraza la Kijeshi la Sudan, Saudia na Imarati zinafuatilia kubakisha hali ya mambo kama ilivyo kwa makusudi ya kulinda maslahi yao katika nchi hiyo ya Kiafrika. Baraza la Kijeshi pia linaona maslahi na uhai wake ukidhaminiwa kupitia kuimarishwa uhusiano na nchi mbili hizo. Hii ni katika hali ambayo makundi yanayolalamika ya Sudan yanataka wanajeshi waondoke madarakani na kuyakabidhi kwa baraza lisilo la kijeshi ambalo litaandaa uchaguzi wa kidemokrasia na kusimamisha uingiliaji wa kigeni katika mambo ya nchi hiyo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa Wasudan wangali wana njia ndefu ya kutembea kabla ya kufikia malengo yao hayo.