Watu wasiopungua 37 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Chad
Watu wasiopungua 37 wameuawa nchini Chad na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kuzuka mapigano mapya ya kikabila.
Vyombo vya usalama vya Chad vinasema kuwa, mapigano hayo mapya ya kikabila yametokea mashariki mwa mkoa wa Ouaddie.
Rais Idriss Deby wa nchi hiyo ametangaza kuwa, mauaji hayo yametokea baada ya kuzuka mapigano makali baina ya wakulima na wafugaji ambayo yalidumu kwa muda wa siku tatu katika mkoa huo unaopakana na nchi jirani ya Sudan.
Akizungumza katika mji mkuu wa nchi hiyo N'Djamena, Rais wa Chad amesema kuwa, mapigano ya kikabila nchini humo yamegeuka na kuwa hangaiko la kitaifa.
Inaeleza kuwa, hii imekuwa ni wiki ya mapigano katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo, na kwamba, hospitali moja imeripoti kuwa watu walipoteza maisha ni 44.
Mbali na mapigano ya kikabila, nchi hiyo inasumbuliwa pia na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram masuala ambayo ni changamoto kubwa kwa serikali ya Chad.
Eneo la Ziwa Chad linapakana na nchi nne za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon. Katika miaka ya hivi karibuni mapigano na vitendo vya uhalifu wa magenge yenye silaha na yenye misimamo mikali kama vile Boko Haram vimeongezeka sana kwenye eneo hilo.