Polisi Zimbabwe yawapiga waandamanaji Harare, yapiga marufuku maandamano dhidi ya serikali
Polisi nchini Zimbabwe leo Ijumaa imetumia gesi ya kutoa machozi na kuwapiga makumi ya wafuasi wa upinzani waliokuwa wameandamana katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo, Harare.
Maandamano hayo yamejiri huku polisi wakitekeleza agizo la kupiga marufuku maandamano dhidi ya serikali ambalo limeungwa mkono na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.
mamia ya wafuasi wa chama cha upinzani cha MDC wamepinga marufuku hiyo na kukabiliana vikali na polisi leo Ijumaa katikati mwa Harare ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya. Polisi aidha iliwakimbiza waandamanaji hao kwa kuwapiga na marungu.
Maandamano haya ya leo katika mitaa ya Harare yamefanyika huku wafuasi wa chama cha upinzani cha MDC wakiituhumu serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa kuwa inachochea machafuko, kufanya ufisadi na kushindwa kusimamia vyema uchumi wa nchi.
Marufuku hiyo ya kufanyika maandamano ya upinzani dhidi ya serikali nchini Zimbabwe ilitangazwa jana jioni na polisi ya nchi hiyo. Hata hivyo Tendai Biti Makamu Mwenyekiti wa chama cha MDC amesema kuwa Katiba ya Zimbabwe inatoa haki kwa kila mtu kufanya maandamano lakini utawala wa kifashisti unawanyima haki hiyo wananchi wa Zimbabwe.
Ameongeza kuwa tangu baada ya mapinduzi ya Novemba 2017 wapinzani wameruka kikaangio na sasa wamekanyaga moto. Amesisitiza kuwa hawatukubaliani na utendaji wa utawala wa Mnangagwa.