SADC yataka Zimbabwe iondolewe vikwazo vya kiuchumi
Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dakta John Pombe Magufuli amesema vikwazo hivyo vimelemaza uchumi wa nchi hiyo.
Rais Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akikabidhiwa uwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na mtangulizi wake Rais Hage Gottfried Geingob wa Namibia, wadhifa ambao ataushikilia kwa mwaka mmoja.
Katika hotuba yake mwenyekiti huo mpya, ameomba rasmi Jamii ya Kimataifa kutathmini upya vikwazo dhidi ya Zimbabwe na kuongezea kuwa nchi hiyo kwa sasa ipo chini ya utawala mpya.
Mwenyekiti huyo mpya ameapa kuhakikisha amani na uthabiti unadumishwa katika kanda hiyo ili kukwamua uchumi wa mataifa wanachama.
Lugha ya Kiswahili pia imetangazwa kuwa lugha ya nne rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Lugha zingine rasmi katika Jumuiya ya SADC ni Kiingereza, Kifaransa na Kireno.
Mkutano huo wa siku 2 unaotarajiwa kumalizika leo Jumapili umewaleta pamoja marais wa nchi 12 pamoja na mawaziri kutoka nchi 16 wanachama.