Makamanda wa jeshi la Algeria waunga mkono uchaguzi wa haraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55772-makamanda_wa_jeshi_la_algeria_waunga_mkono_uchaguzi_wa_haraka
Mkuu wa Jeshi la Algeria kwa mara nyingine ameunga mkono kufanyika uchaguzi wa rais haraka iwezekanavyo nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 03, 2019 03:36 UTC
  • Makamanda wa jeshi la Algeria waunga mkono uchaguzi wa haraka

Mkuu wa Jeshi la Algeria kwa mara nyingine ameunga mkono kufanyika uchaguzi wa rais haraka iwezekanavyo nchini humo.

Mtandao wa habari wa al Nahar umenukuu Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah, (Mkuu wa Jeshi la Algeria) akitoa mwito wa kuitishwa kikao cha kamati ya uchaguzi, tarehe 15 mwezi huu wa Septemba ili kuainisha muda wa kufanyika uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Amesema, kuna ulazima wa kufanyiwa marekebisho sheria ya uchaguzi ili iendane na mazingira ya hivi sasa ya Algeria.

Maandamano ya wananchi wa Algeria ya kushinikiza kufukuzwa serikali mabaki ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika

 

Hata hivyo wapinzani wa serikali ya hivi sasa ya Algeria wamepinga mpango na mbinu zinazotumiwa na jeshi za kuitisha uchaguzi haraka na wanataka kufanyike mabadiliko ya kimsingi ya katiba na ya sheria ya uchaguzi ndipo ufanyike uchaguzi huo.

Kinachosisitizwa zaidi hivi sasa na wananchi wa Algeria waliofanya mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Rais Abdulaziz Bouteflika, ni kufukuzwa serikalini mabaki yote ya utawala huo uliopinduliwa na wananchi, akiwemo mkuu mwenyewe wa jeshi, Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah pamoja na Waziri Mkuu wa hivi sasa wa Algeria,  Noureddine Bedoui.

Ijumaa ya kila wiki wananchi wa Algeria wanaendelea kufanya maandamano ya nchi nzima kushinikiza kutekelezwa kivitendo matakwa yao.