Rais wa Algeria atoa wito wa kuundwa tume huru ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55908-rais_wa_algeria_atoa_wito_wa_kuundwa_tume_huru_ya_uchaguzi
Rais wa muda wa Algeria ametoa wito wa kufanyika mashauriano kwa ajili ya kuunda tume huru ya uchaguzi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2019 22:08 UTC
  • Rais wa Algeria atoa wito wa kuundwa tume huru ya uchaguzi

Rais wa muda wa Algeria ametoa wito wa kufanyika mashauriano kwa ajili ya kuunda tume huru ya uchaguzi nchini humo.

Abdel Qadir bin Saleh amesema kuwa, serikali imetekeleza ahadi yake ya kutoingilia mwenendo wa mazungumzo ya kitaifa ambayo yamekurubisha pamoja mitazamo mbalimbali kuhusiana na udharura wa kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo haraka iwezekanavyo. 

Bin Saleh pia ameeleza kuridhishwa kwake na kuwepo uhuru na uwazi vinavyotayarisha mazingira mazuri ya kufanyika mazungumzo ya kitaifa baada ya kupokea ripoti ya mwisho ya Kamisheni ya Taifa ya Upatanishi na Mazungumzo iliyotayarishwa na vyama vya siasa, wawakilishi wa jumuiya za kiraia, viongozi wa kitaifa na harakati za wananchi wa Algeria.

Maandamano Algeria

 

Siku ya Jumapili Jukwaa la Taifa la Mazungumzo lililopewa jukumu la kuiondoa Algeria katika mgogoro wa kisiasa lilimkabidhi Rais wa muda wa nchi hiyo ripoti yake ya mwisho na kutoa wito wa kuitishwa uchaguzi wa rais haraka iwezeknavyo. 

Tangu baada ya kujiuzulu aliyekuwa rais wa Algeria, Abdel Aziz Bouteflika tarehe 2 Aprili mwaka huu, Waalgeria wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kufutwa kazi maafisa wa  kipindi cha utawala wake waliosalia madarakani.

Uchaguzi wa rais wa Algeria ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 4 Julai lakini uliahirishwa hadi wakati mwingine baada ya kutojitokeza mgombea hata mmoja.