Algeria yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais
Rais wa mpito wa Algeria ametangaza Disemba 12 kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo.
Abdel Qadir Bin Saleh amewaomba wananchi wa Algeria kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la kidemokrasia. Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, rais huyo wa muda amesema, "Nimesaini dikrii ya kufanyika uchaguzi mnamo Disemba 12 mwaka huu. Ninakuombeni mjitokeze kwa wingi."
Amebainisha kuwa, uchaguzi ndilo chaguo pekee linaloweza kuikwamua nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwenye mgogoro unaoikabili.
Amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itashirikiana na vyombo husika vya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa njia huru, ya uwazi na haki.
Tangu baada ya kujiuzulu aliyekuwa rais wa Algeria, Abdel Aziz Bouteflika tarehe 2 Aprili mwaka huu, Waalgeria wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kufutwa kazi maafisa wa kipindi cha utawala wake waliosalia madarakani.
Uchaguzi wa rais wa Algeria ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 4 Julai lakini uliakhirishwa baada ya kutojitokeza mgombea hata mmoja.