Mugabe azikwa katika kijiji alikozaliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56316-mugabe_azikwa_katika_kijiji_alikozaliwa
Kiongozi mwanzilishi wa taifa la Zimbabwe Robert Mugabe amezikwa Jumamosi katika kijiji alikozaliwa cha Kutama katika eneo la Zvimba na hivyo kuhitimisha mgogoro baina ya serikali na mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa kuhusu sehemu yake ya kuzikwa.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Sep 29, 2019 07:49 UTC
  • Mugabe azikwa katika kijiji alikozaliwa

Kiongozi mwanzilishi wa taifa la Zimbabwe Robert Mugabe amezikwa Jumamosi katika kijiji alikozaliwa cha Kutama katika eneo la Zvimba na hivyo kuhitimisha mgogoro baina ya serikali na mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa kuhusu sehemu yake ya kuzikwa.

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe aliaga dunia Septemba 6 mwezi huu huko nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu.

Awali, serikali ilikuwa imesema Mugabe angezikwa katika makaburi ya mashujaa jijini Harare. Uamuzi huo wa serikali ulikataliwa na familia ya hayati Mugabe. Waziri wa Habari nchini humo Nick Mangwana amesema katika taarifa kwamba, serikali imeona ni vema itii matakwa ya familia kuhusu ni wapi mpendwa wao azikwe.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Mugabe ambaye aliiongoza Zimbabwe kwa karibu miongo minne tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 alilazimishwa kujiuzulu mwezi Novemba mwaka juzi baada ya mapinduzi ya jeshi.

Mugabe alikuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe na kuiondoa nchi hiyo katika makucha ya mkoloni na hata baada ya uhuru wa Zimbabwe, alisimama kidete kutetea mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.