Apr 23, 2016 06:35 UTC
  • Ban amtaka Machar kurejea Juba

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemtaka kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Rieck Machar arejee katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.

Ban Ki-moon amemtaka Rieck Machar kurejea Juba bila ya masharti yoyote kwa mujibu wa mapatano ya amani ya pande hasimu nchini Sudan Kusini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, ni muhimu sana kulinda roho ya ushirikiano kwa ajili ya kujenga upya uharibifu uliosababishwa na mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini.

Rieck Machar alitarajiwa kwenda katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa kama Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir. Kwa sasa Machar yuko katika kambi ya Pagak iliyopo katika mpaka wa Sudan Kusini na Ethiopia.

Hitilafu zilizojitokeza baina ya serikali ya Sudan Kusini na wapinzani zimechelewesha kurejea kwa Machar mjini Juba. Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake juu ya kucheleweshwa utekelezaji wa makubliano ya amani nchini Sudan Kusini.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Tags