Oct 05, 2019 02:39 UTC
  • Maelfu watiwa nguvuni Misri katika maandamano yanayomtaka al Sisi ang'atuke

Kamisheni ya Haki na Uhuru ya Misri imetangaza kuwa, askari usalama wa nchi hiyo wamewatia nguvuni raia zaidi ya elfu 3 katika maandamano ya wiki mbili za hivi karibuni dhidi ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi huyo.

Takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Haki na Uhuru ya Misrii zinasema kuwa, watu 3080 walioshiriki katika maandamano ya kumtaka al Sisi ang'atuke madarakani wametiwa nguvuni kuanzia tarehe 20 mwezi uliopita wa Septemba na kwamba, mji wa Cairo ndio uliokuwa na idadi kubwa zaidi ya raia waliotiwa nguvuni ukifiatiwa na Suez, Alexandria na mikoa mingine. 

Taasisi hiyo iimesema, kuna makumi ya waandamanaji wengine waliotiwa nguvuni na vyombo vya usalama vya Misri ambao familia zao hazikutaka kutoa ripoti zao kwa taasisi za kutetea haki za binadamu. 

Taasisi 9 za kutetea haki za binadamu za Misri Jumatano wiki hii zilikosoa vikali ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi dhidi ya wapinzani wake hususan kamatakamata inayofanywa dhidi ya waandishi wa habari, wanasheria na viongozi wa vyama vya siasa. 

Miji mbalimbali ya Misri imekuwa uwanja wa maandamano makubwa yanayomtaka Rais wa nchi hiyo jenerali mstaafu Abdel Fattah al Sisi aondoke madarakani. Maandamano hayo yanafanyika kutokana na wito wa Muhammad Ali anayeishi uhamishoni nchini Uhispania ambaye ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa serikali ya al Sisi.

Kabla ya kukimbilia nje ya nchi, Muhammad Ali alikuwa mkandarasi wa jeshi la Misri na amefichua jinsi kiongozi wa sasa wa nchi hiyo anavyopora mali ya umma na kujitajirisha yeye, familia na majenerali wa jeshi kwa kujenga majumba na makasri ya kifahari.  

Tags