Misri: Mashambulio ya Uturuki dhidi ya Syria ni tishio kwa Waarabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56583-misri_mashambulio_ya_uturuki_dhidi_ya_syria_ni_tishio_kwa_waarabu
Sameh Shoukry, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri amesema kuwa, mashambulio ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria yanakiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na ni tishio kwa nchi za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2019 22:54 UTC
  • Misri: Mashambulio ya Uturuki dhidi ya Syria ni tishio kwa Waarabu

Sameh Shoukry, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri amesema kuwa, mashambulio ya kijeshi ya Uturuki dhidi ya Syria yanakiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na ni tishio kwa nchi za Kiarabu.

Sameh Shoukry, amesema hayo katikka mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) huko Cairo Misri na kueleza kwamba, mashambulio ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria ni kufungua ukurasa mpya wa hatua zilizo dhidi ya mamlaka ya kujitawala mataifa ya dunia.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri ameongeza kuwa, Syria ina haki ya kusimama na kukabiliana na mashambulio hayo na kwamba, serikali ya Ankara inabeba dhima ya kurejea makundi ya kigaidi katika eneo.

Jumatano iliyopita, Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki alitangaza kuanza oparesheni ya kijeshi ya nchi yake kwa jina la "Chemchemi ya Amani" dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi huko kaskazini mwa Syria licha ya operesheni hiyo kupingwa kimataifa. 

Raia wa Syria wakikimbia mashambulizi ya Uturuki

Taasisi mbalimbali za kimataifa zimetahadharisha kuhusu taathira mbaya za mashambulizi ya Uturuki kaskazini mwa Syria na kutangaza kuwa mashambulizi hayo yanaweza kusababisha mamia ya watu kuwa wakimbizi.

Wakati huo huo, viongozi wa Syria wamesisitiza kuwa Wasyria watalinda na kutetea ardhi yote ya nchi yao. Kwa upande wao wapiganaji wa Kikurdi wanaojiita Syrian Democratic Forces (SDF) wametangaza kuwa, watayageuza mashambulizi ya jeshi la Uturuki kuwa vita haribifu dhidi ya nchi hiyo.