AU, SADC zataka Marekani na EU kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56878-au_sadc_zataka_marekani_na_eu_kuondoa_vikwazo_dhidi_ya_zimbabwe
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameunga mkono wito wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa kutaka Zimbabwe iondolewe bila masharti vikwazo ambavyo imewekewa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 27, 2019 03:18 UTC
  • AU, SADC zataka Marekani na EU kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameunga mkono wito wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa kutaka Zimbabwe iondolewe bila masharti vikwazo ambavyo imewekewa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya.

Faki amesema vikwazo hivyo vya Wamagharibi vimekuwa na taathira mbaya kwa nchi nzima ya Zimbabwe.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC nayo imesisitiza tena wito wake wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Zimbabwe.

Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo Lawrence Tax ametoa taarifa ikisema, kuondolewa vikwazo hivyo kutawanufaisha watu wa Zimbabwe, kanda ya SADC kwa ujumla na ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na Marekani.

Vikwazo hivyo vilivyowekwa mwaka 2002 na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya, ambavyo ni pamoja na vizuizi vya kibiashara na kifedha, vinakadiriwa kuigharImu Zimbabwe karibu dola bilioni 100 za Kimarekani.

 

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Siku ya Ijumaa maelfu ya wananchi wa Zimbabwe waliandamana wakitaka Marekani na Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo vya 'kishetani' dhidi ya rais wa nchi hiyo na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.

Waandamanaji waliokuwa na hasira walijumuika katika Medani ya Robert Mugabe mjini Harare kabla ya kuelekea katika Uwanja wa Kitaifa na kuhutubiwa na Rais Emmerson Mnangagwa ambaye alilaani vikali vikwazo hivyo.