Sudan yaakhirisha mazungumzo na makundi ya waasi
(last modified Wed, 20 Nov 2019 06:57:26 GMT )
Nov 20, 2019 06:57 UTC
  • Sudan yaakhirisha mazungumzo na makundi ya waasi

Serikali ya Sudan imekubali ombi mla kuakhirisha hadi mwezi ujao mazungumzo ya amani kati yake na makundi ya waasi wanaobeba silaha yaliyotazamiwa kufanyika kesho Alkhamisi kufuatia ombi la timu ya wapatanishi.

Mohamed Al-Hassan Al-Taishi, msemaji wa Baraza Kuu la Amani la Sudan amesema duru mpya ya mazungumzo hayo ya amani kati ya serikali ya Khartoum na makundi yenye silaha kutoka majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile itafanyika Disemba 10 katika nchi jirani ya Sudan Kusini.

Oktoba 14, Juba mji mkuu wa Sudan Kusini ilikuwa mwenyeji wa duru nyingine ya mazungumzo ya amani kati ya serikali na makundi ya waasi.

Wiki moja baadaye, Jeshi la Sudan lilisema kuwa kundi la waasi la SLM limekiuka mapatano ya kusitisha vita yaliyotangazwa baina ya pande hasimu nchini humo na limewashambulia wanajeshi wa serikali.

Serikali mpya inayoongozwa na Hamdok ikiapishwa

Mazungumzo hayo ya amani yanafanyika kufuatia mwito wa nchi za eneo kwa pande hizo kuonyesha nia ya kisiasa ya kutatua mgogoro ambao umekuwa ukitokota nchini humo kwa muda mrefu.

Sudan imejipa miezi sita kufikia mkataba kamili wa amani. Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Sudan, Abdallah Hamdok amesema kupata amani ya kudumu ni kipaumbele cha serikali anayoiongoza.