Polisi Algeria yawatia mbaroni makumi ya watu wanaopinga kufanyika uchaguzi wa rais
Askari usalama nchini Algeria wamewatia mbaroni watu wasiopungua 30 wanaopinga kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo. Watu hao wamekamatwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Algiers.
Alhamisi iliyopita pia askari usalama wa Algeria waliwatia nguvuni watu wasiopungua 80 ambao walishiriki kwenye maandamano ya kupinga kufanyika uchaguzi huo.
Wafanya maandamano hao wanasisitiza kuwa kabla ya kufanyika uchaguzi wowote ule viongozi wa zama za utawala wa Rais Abdulaziz Bouteflika wanapaswa kuondoka madarakani. Shakhsia kama Abdulmajid Tabu'n na Ali Benflis Mawaziri Wakuu wa zamani wa Algeria, Izzudin Mihoubi Waziri wa zamani wa Utamaduni, Abdulqaher bin Qareena Waziri wa zamani wa Sheria na Abdulaziz Bilid Mkuu wa chama cha Harakati ya al Mustaqil wanaonekana katika orodha ya mwisho ya Tume ya Uchaguzi ya Algeria.
Wananchi wa Algeria wanataka kufanyika marekebisho ya msingi nchini humo. Maandamano yalianza kushuhudiwa huko Algeria mara baada ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Abdulaziz Bouteflika kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tano mtawalia. Maandamano hayo hatimaye yalipelekea kuuondoka madarakani Bouteflika.