Madaktari wanaogoma Zimbabwe wakataa nyongeza ya mshahara
Madaktari wanaoendelea na mgomo nchini Zimbabwe tokea mwezi Septemba mwaka huu wamekataa pendekezo la serikali la kurejea kazini baada ya kupewa nyongeza ya mishahara.
Kwa mujibu wa Muungano wa Madaktari wa Hospitali za Zimbabwe ( ZHDA), serikali imesema kima cha juu cha nyongeza inachoweza kuwapa madaktari hao ni dola 3,900 za Zimbabwe, sawa na dola 240 za Marekani kwa mwezi. Hata hivyo madaktari wa Zimbabwe hawakubaliani na nyongeza hiyo.
Madaktari hao waliamua kufanya mgomo ili kushinikiza kuboreshwa mazingira ya kazi na kupandishiwa mishahara yao kutokana na kupanda kwa gharama za maisha. Baadhi ya madaktari nchini humo wanalipwa chini ya dola 100 za Marekani kwa mwezi.
Siku ya Alkhamisi, serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo iliwataka madaktari warejee kazini ndani ya masaa 48, vinginenevyo wapigwe kalamu nyekundu. Tayari serikali ya Harare imewafuta kazi madaktari 448 wa nchi hiyo kwa kushiriki mgomo, huku ikitishia kuwachukulia hatua za kinidhamu wengine zaidi ya 1,000.
Hata kabla ya kuanza mgomo wa madaktari mwezi Septemba mwaka huu, aghalabu ya hospitali za umma nchini Zimbabwe zilikuwa zinakabiliwa na uhaba wa dawa na suhula muhimu za matibabu.
Zimbabwe inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi kwa miaka kadhaa sasa, ambapo vikwazo vya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani vimetajwa kushadidisha hali hiyo.