Maelfu ya Waalgeria waandamana baada ya rais mpya wa nchi hiyo kuapishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58012-maelfu_ya_waalgeria_waandamana_baada_ya_rais_mpya_wa_nchi_hiyo_kuapishwa
Makumi ya maelfu ya watu waliandamana jana nchini Algeria baada ya Sala ya Ijumaa kupinga kuchaguliwa rais mpya wa nchi hiyo Abdelmajid Tebboune, ambaye tayari ameshatawazwa kushika wadhifa huo, huku harakati ya umma iliyopinga kufanyika uchaguzi wa rais ikitafakari wito wa kufanya mazungumzo uliotolewa na kiongozi huyo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 21, 2019 04:09 UTC
  • Maelfu ya Waalgeria waandamana baada ya rais mpya wa nchi hiyo kuapishwa

Makumi ya maelfu ya watu waliandamana jana nchini Algeria baada ya Sala ya Ijumaa kupinga kuchaguliwa rais mpya wa nchi hiyo Abdelmajid Tebboune, ambaye tayari ameshatawazwa kushika wadhifa huo, huku harakati ya umma iliyopinga kufanyika uchaguzi wa rais ikitafakari wito wa kufanya mazungumzo uliotolewa na kiongozi huyo.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera ya taifa walikuwa wakitoa nara na kaulimbiu za "Tebboume si rais wetu" na "tutaendeleza maandamano ya upinzani" huku wakipita kwenye mtaa mkuu wa mji mkuu Algiers uliokuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Waandamanaji wengine walipaza sauti zao wakisema: "Polisi ni wasaliti", "hatutofanya mazungumzo na watu waongo" na "hatutarudi nyuma", sambamba na kutoa wito kwa wenzao katika mji wa magharibi wa Oran, ambako kuna taarifa za watu kutiwa nguvuni, waendeleze maandamano.

Maandamano hayo ya jana yamefanyika baada ya kupita wiki moja tangu ulipofanyika uchaguzi wa rais na kuchaguliwa Abdelmajid Tebboune kuwa rais mpya wa Algeria.

Rais mpya wa Algeria, Abdelmajid Tebboune

Baada ya kuapishwa siku ya Alkhamisi, Tebboune alitoa wito wa mazungumzo na waandamanaji, akiahidi kufuatilia kwa haraka mchakato wa mabadiliko ya katiba itakayoweka kikomo cha mihula miwili ya urais.

Kutokana na harakati ya umma kutokuwa na uongozi rasmi, baadhi ya shakhsia mashuhuri wanaoiunga mkono wameshauri yafanyike mazungumzo na serikali mpya, hata hivyo waandamanaji hapo jana walisisitiza kuwa hawatozungumza na mtu wanayeamini kuwa ni kibaraka wa utawala uliopita.

Maandamano ya upinzani nchini Algeria, yamekuwa yakifanyika kila Ijumaa tangu mwezi Februari, kutaka maafisa wote wakuu wa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika waondoke madarakani, ukomeshwe ufisadi na jeshi lisijihusishe na siasa.

Aliyekuwa rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika

Licha ya upinzani mkali wa wananchi, uchaguzi wa rais wa Algeria ulifanyika tarehe 12 Desemba kwa uungaji mkono wa asasi na shakhsia wenye mfungamano na utawala wa Bouteflika, ambapo Abdelmajid Tebboune aliibuka mshindi kwa kujipatia asilimia 58.13 ya kura huku duru rasmi za serikali zikitangaza kuwa ni asilimia 40 tu ya waliotimiza masharti walijitokeza kupiga kura.

Wananachi wanaopinga uchaguzi huo wanasema, wagombea wote waliopitishwa kuwania urais wana mfungamano na serikali ya Abdelaziz Bouteflika.

Algeria ilishuhudia wimbi kubwa la maandamano ya umma kuanzia mwezi Februari, baada ya Bouteflika kutangaza uamuzi wa kugombea tena urais kwa muhula wa tano mfululizo. Hatimaye kutokana na mashinikizo hayo ya umma, mnamo mwezi Aprili, kiongozi huyo aliyeitawala Algeria kwa muda wa miaka 20 alisalimua amri kwa matakwa ya umma na kung'atuka madarakani.../