WFP: Zimbabwe inakabiliwa na hatari ya baa kubwa la njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58223-wfp_zimbabwe_inakabiliwa_na_hatari_ya_baa_kubwa_la_njaa
Zimbabwe inakabiliwa na hatari ya baa kubwa la njaa ambapo karibu watu milioni 8 sawa na nusu ya watu wote wa nchi hiyo hawana uhakika wa chakula.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 31, 2019 13:00 UTC
  • WFP: Zimbabwe inakabiliwa na hatari ya baa kubwa la njaa

Zimbabwe inakabiliwa na hatari ya baa kubwa la njaa ambapo karibu watu milioni 8 sawa na nusu ya watu wote wa nchi hiyo hawana uhakika wa chakula.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mamilioni ya Wazimbabwe wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na ukame wa muda mrefu na mgogoro wa kiuchumi. WFP imetoa wito wa uwekezaji wa haraka ili kuongeza mara mbili idadi ya watu inayowasaidia na kuonya kuwa misaada isipopatika, wananchi wa Zimbabwe watakumbwa na hali mbaya sana.

WFP inataka kuongeza idadi ya watu wanaopokea msaada mara mbili hadi kufikia milioni 4.1 na ili kuweza kufanya hivyo inahitaji zaidi ya dola milioni 200 katika nusu ya kwanza pekee ya mwaka 2020. Niels Balzer, naibu mkurugenzi wa WFP nchini Zimbabwe anasema  mwaka 2019 umekuwa mgumu sana kwa Wazimbabwe wote.  Amesema sababu za matatizo ya Zimbabwe ni mdororo wa kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, na ukame mkali ambao umesababisha zaidi ya watu milioni 8 kutokuwa na uhakika wa chakula.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Ameongeza kuwa miaka mingi ya ukame imepunguza uzalishaji wa chakula Zimbabwe kwa kiasi kikubwa nchi ambayo awali ilijulikana kama kapu la mkate barani Afrika. Mavuno ya mahindi yalipungua kwa asilimia 50 mwaka 2018, na kufikia Agosti 2019 WFP ililazimika kuzindua msaada wa dharura ili kukidhi mahitaji yaliyoongezeka  mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Msimu huu kwa mujibu wa WFP mvua zimechelewa tena na hazitoshi kwa kilimo huku mbegu nyingi zilizopandwa hazijaoota hivyo utabiri unaonyesha kwamba kutakuwa na muendelezo wa jua kali na ukame, vikiashiria mavuno duni mwezi Aprili na hivyo kuyaweka maisha ya mamilioni ya watu na mifugo katika hatari kubwa