Jan 24, 2020 02:53 UTC
  • Angola kutoa waranti ya kukamatwa binti 'fisadi' wa rais wa zamani

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Angola amesema ikilazimu, serikali ya nchi hiyo itatoa waranti ya kimataifa ya kukamatwa na kurejeshwa nchini humo mfanyabiashara bilionea na binti wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jose Eduardo dos Santos.

Helder Pitta Gros amesema kwa sasa wanatoa mwito kwa bilionea huyo na watuhumiwa wengine wa ufisadi wa kifedha kurejea kwa khiari nchini ili wafunguliwe mashitaka, vinginevyo serikali itatoa waranti za kukamatwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Angola (Angop), Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Angola jana Alkhamisi akiwa mjini Lisbon alizungumzia kuhusu uwezekano wa kutolewa waranti hizo za kukamatwa na kurejeshwa nchini watuhumiwa hao wa ufisadi akiwemo Isabel dos Santos, binti wa rais wa zamani wa nchi hiyo.

Siku ya Jumapili, vyombo kadhaa vya habari vya ndani na nje ya Angola vilichapisha mamia ya maelfu ya nyaraka zilizofichuliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari Wapekuzi (ICIJ) kuhusu namna Isabel dos Santos alivyofyonza utajiri wa nchi hiyo, wakati babake akiwa rais.

Rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos

Isabel dos Santos aliye na umri wa miaka 46 na ambaye sehemu kubwa ya utajiri wake ipo katika nchi za Ulaya na Imarati, amekuwa akikanusha tuhuma dhidi yake akisema hazina msingi wowote.

Isabel dos Santos alihama Angola baada ya baba yake, Jose Eduardo dos Santos aliyetawala nchi hiyo kwa karibu miaka 40, kuondoka madarakani mwaka 2017 na nafasi yake kuchukuliwa na Joao Lourenco. 

 

Tags