UN: Tunahitaji dola milioni 76 kupambana na nzige waliovamia Afrika Mashariki
(last modified Fri, 31 Jan 2020 02:42:06 GMT )
Jan 31, 2020 02:42 UTC
  • UN: Tunahitaji dola milioni 76 kupambana na nzige waliovamia Afrika Mashariki

Umoja wa Mataifa umesema unahitaji dola milioni 76 haraka iwezekanavyo za kudhibiti mlipuko wa nzige wa jangwani waliovamia baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Dominique Bourgeon, Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari mjini Rome, Italia na kubainisha kuwa, kwa sasa wamefanikiwa kukusanya dola milioni 15 tu za kupambana na wadudu hao wanaovamia mimema na mashamba ya kilimo.

Amesema kusambaa kwa nzige hao ambako hakujashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 70 kutasababisha hali ya baa la njaa ambalo tayari linakabili mamilioni ya raia wa Kenya, Ethiopia na Somalia kuwa mbaya zaidi.

Afisa huyo wa FAO amesema sehemu kubwa ya fedha hizo inapaswa kutumika kwa ajili ya operesheni ya kupuliza dawa ya kuua nzige hao.

Nzige katika shamba la kilimo kaskazini mashariki mwa Kenya

Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, idadi ya nzige hao itaongezeka mara 500 zaidi.

Mlipuko huo wa nzige wa jangwani umeripotiwa kuwa miongoni mwa athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Tags