Apr 29, 2016 07:09 UTC
  • Kaburi la umati la Mashia Nigeria laoneshwa na Televisheni ya Ufaransa

Televisheni ya Ufaransa imeonesha picha za kaburi la umati la Waislamu wa madhehebu ya Shia waliouawa kinyama mwishoni mwa mwaka jana na jeshi la Nigeria.

Taarifa hiyo ya Televisheni ya Ufaransa inaonesha kuwa, kuna kaburi la umati la Waislamu wa Kishia kando kando ya mji wa Kaduna. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Waislamu wa Kishia 350 wa Nigeria wakiwemo wanawake na watoto wadogo wamezikwa katika kaburi hilo la umati.

Ripoti hiyo aidha inaeleza kuwa, serikali ya kieneo ya Kaduna imethibitishwa kwamba, watu 347 walizikwa katika eneo hilo. Baadhi ya ripoti zinasema, idadi ya watu waliuawa katika eneo hilo katika shambulio la jeshi Disemba mwaka jana ni kubwa zaidi.

Ripoti hiyo inakuja siku chache tu baada ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International kutangaza kuwa, jeshi la Nigeria liliua zaidi ya Waislamu 350 wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky Disemba mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa, Disemba 12 mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika kituo cha Kiislamu cha mji wa Zaria baada ya kuwatuhumu kuwa walifunga njia ya msafara wa mkuu wa jeshi kwa njama ya kutaka kumuua.

Tags