Jeshi la Chad laua wapiganaji elfu moja wa Boko Haram
Msemaji wa jeshi la Chad ametangaza kuwa jeshi hilo limewaangamiza magaidi elfu moja wa kundi la Boko Haram huko Magharibi mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi la Chad, Azem Bermendoa Agouna amesema kuwa katika operesheni hiyo ya kusafisha maeneo yote ya Chad, wapiganaji elfu moja wa Boko Haram wameuawa katika kipindi cha wiki moja. Ameongeza kuwa askari 52 wa nchi hiyo pia wameuawa katika operesheni hiyo.
Agouna amesema operesheni hiyo, ambayo ilizinduliwa baada ya askari karibu 100 kuuawa katika shambulio la Boko Haram mwezi uliopita, ilimalizika Jumatano baada ya wapiganaji wenye silaha kufukuzwa nje ya nchi.
Taarifa hii ya jeshi la Chad ni ya kwanza rasmi ya matokeo ya Operesheni ya Hasira za Bohoma, iliyozinduliwa baada ya askari 92 kuuawa mnamo Machi 23 katika shambulio kubwa zaidi la Boko Haram dhidi ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo. Kundi hilo lilishambulia kambi ya jeshi ya Bohoma kwa masaa saba na kuua idadi hiyo ya wanajeshi.
Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake mwaka 2009 nchini Nigeria na tangu mwaka 2015 lilipanua zaidi hujuma zake hadi katika nchi jirani kama Chad, Niger na Cameroon.