Misiri yaongeza muda wa hali ya hatari kwa miezi mitatu
(last modified Tue, 28 Apr 2020 11:11:04 GMT )
Apr 28, 2020 11:11 UTC
  • Misiri yaongeza muda wa hali ya hatari kwa miezi mitatu

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri leo ametangaza kuwa hali ya hatari kitaifa nchini humo itaendelea kwa muda wa miezi mingine mitatu.

Katika dikrii yake, al-Sisi ametetea uamuzi wake kwa kusema kuwa, nchi hiyo sasa inakabiliwa na hatari kutokana na hali katika sekta za afya na usalama.

Sheria ya hali ya hatari inawawezesha watawala wa Misri kuchukua hatua maalumu ikiwa ni pamoja na kuwafikisha washukiwa wa ugaidi katika mahakama za kijeshi, kutekeleza sheria za kutotoka nje na kubana yanayoandikwa katika magazeti.

Mbali na ugaidi, Misri pia inakabiliana na ugonjwa wa corona ambao umepelekea watu zaidi ya 200,000 kupoteza maisha duniani.

Jumatatu 27 Aprili Wizara ya Afya ya Misri ilisema idadi ya watu walioambukizwa corona nchini humo ni 4,782 ambapo 337 wamefariki dunia.

Hujuma ya kigaidi nchini Misri

Serikali ya Misri imetangaza sheria ya kutotoka nje usiku pamoja na hatua zingine kadhaa ili kuzuia kuenea corona. Wakuu wa Misri wamefunga shule, vyuo vikuu, misikiti, makanisa na vituo vya utalii ikiwa ni katika mkakati wa kuzuia kuenea corona. Hata hivyo maduka yanafunguliwa kila siku hadi saa 11 jioni katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Rais wa hivi sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi aliingia madarakani mwaka 2013 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Mohammad Morsi, rais pekee aliyewahi kuchaguliwa kidemokrasia huko nchini Misri.

Tangu wakati huo hadi hivi sasa Abdel Fattah el Sisi anaendelea kuwakandamiza kikatili wapinzani kwa uungaji mkono kamili wa baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Saudi Arabia.

 

Tags