Wamalawi kushiriki uchaguzi wa rais wa marudio kesho Jumanne
Wananchi wa Malawi wanatazamiwa kuelekea katika masanduku ya kupigia kura kesho Jumanne kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa urais wa marudio.
Uchaguzi huo wa marudio ambao unakuja miezi 13 baada ya wananchi wa Malawi kushiriki uchaguzi mwingine mkuu mwezi Mei mwaka jana 2019, unatazamiwa kufanyika licha ya janga la corona ambalo limeshaua watu 11 kufikia sasa, mbali na kesi 730 za maradhi hayo kuripotiwa nchini humo.
Uchaguzi huo unarejewa baada ya Mahakama ya Katiba nchini humo kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Mei 2019 yaliyompa ushindi Rais Peter Mutharika mwenye umri wa miaka 80.
Awali Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Malawi, Jane Ansah alitangaza kuwa uchaguzi huo wa marudio ungefanyika Julai Pili mwaka huu kufuatia uamuzi huo wa mahakama.

Mahakama ya Katiba ya Malawi mnamo Februari 3 mwaka huu ilifuta matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 2019 na kuagiza kufanyika uchaguzi mpya kwa sababu ya udanganyifu, dosari na kasoro nyingi zilizoshuhudiwa katika zoezi hilo.
Rais Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP) atachuana na kinara wa chama cha upinzani cha Malawi Congress Party (MCP), Lazarus Chakwera, mwenye umri wa miaka 65, huku mgombea mwingine ambaye hafahamiki sana miongoni mwa Wamalawi, Peter Kuwani akijitosa pia katika kinyang'anyiro hicho.